WAKUNYAKU
Mpole ukimuona, mwenye machache maneno,
Suti yake ya kushona, hakika haina mfano,
Warembo wakikutana, wamsema mkutano,
Jina lake Wakunyaku, yeyote ananyakua,
Amehama makanisa, hili sasa ni la saba,
Awamaliza vipusa, hata kwa zake hotuba,
Huyu ndugu anatesa, roho yake ya kahaba,
Jina lake Wakunyaku, yeyote anachukua,
Recho yule wa kwaya, Wakunyaku kamtwaa,
Siku hizi bila haya, wanatembea kwa mtaa,
Amtumia vibaya, na wala hatamuoa,
Jina lake Wakunyaku, yeyote anachukua,
Kuwawadia wageni, Wakunyakui namba wani,
Binti akiwa mgeni, ashamueka simuni,
Kesho yupo naye ndani, shamtoa kanisani,
Jina lake Wakunyaku, yeyote anachukua,
Yule mama wa fulani, aketiye katikati,
Walimuona njiani, na Wakunyaku wameketi,
Ni mama wa kanisani, na wanaitana switi,
Jina lake Wakunyaku, yeyote anachukua,
Kwenye maombi ya kesha, Wakunyaku hatakosa,
Anawatia puresha, wadada kwenye kanisa,
Anakitu chamuwasha, lazima tu atagusa,
Jina lake wakunyaku, yeyote ananyakua,
Kila kanisa nchini, halikosi Wakunyaku,
Iwapo hayupo ndani, basi yuko 'nje huku,
La, sio wewe jamani, naomba usijishuku,
Jina lake Wakunyaku, yeyote anachukua,
Sasa ni mda mwafaka, swala hili kuombea,
Tuliombee haraka, na pia kulikemea,
Tusije kuabika, kisa tumelipuzia,
Jina lake Wakunyaku, yeyote anachukua,
Green Ruwa
Mtoto wa Gwiji
No comments:
Post a Comment