Tuesday, October 10, 2023

KUMBUKUMBU

KUMBUKUMBU
 
Kilichofanyika kwangu, kimefunza hakika

Kuishi na walimwengu, ni utu na kadhalika,

Yote tumuachie Mungu, yatosha tulipofika,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Nikisha kusimulia, huruma tanionea,

Majina utanipea, Kwa yale nilopitia,

Nikweli sikusikia, ya baba alonambia,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Wema ulinitongea, nikajipata pabaya,

Kwa kweli sikudhania, yatanitokea haya,

Amini nilikusaidia, yote kumpatia,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Hadithi, hadithi njoo…Lakini hutoamini,

Tuache hadithi hio, sijui niseme nini,

Kidogo tena sikia, tuchambue jaladani,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Hua ni giza totoro, kile usichokijua,

Hakuonyesha kasoro, pale tulipoanzia,

Ningeina tumoro,Ruwa ningelikimbia,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Nimetamani kuchora, yote niloyapitia,

Yamejaa kwa fikira, yamejaa kwa hisia,

Mengine yananikera, mengine yanisumbua,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Nitachora siku moja, iwe kama ya filamu,

Kwa sasa, naomba, ngoja, tuitayarishe hamu,

Ili tunapoitaja, iwe tunaifahamu,

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Duizo nimezikwepa, nakiri kutorudia,

Sirudii ninaapa, nitaishi kungojea,

Mola wangu atanipa, heri sasa kungojea

Nina kumbukumbu nzuri, nina kumbukumbu mbaya.

Green Ruwa

Mtoto Wa Gwiji 

No comments:

BINTI YETU

BINTI YETU Ni heri basi arudi, kuliko kututesea, Kwa sasa hatuna budi, sisi kama familia, Hizo dhiki zimezidi, mrudishe twakwambia, Binti ye...