MWAKA HUU SIKOPI!
Kwanza Rabana asante, tarehe mosi mefika,
Yalopita sinikute, ya mwaka jana mashaka,
Lazima pesa nipate, kukopa nimeshachoka,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
Nilikopa pasi utu, kuziba vyangu viraka,
Wakanilaumu watu, kwa kuwakopa haraka,
Naapa sitosubutu, kukukopa ewe kaka,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
Shida zilikua nyingi, shingoni yalinifika,
Kukopa hio shilingi, sikupenda kwa hakika,
Mwaka huu pesa nyingi, walai ntazishika,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
Wengine walinyamaza, kunipa hawakutaka,
Naapa nitajikaza, mambo haya kuepuka,
Si uongo yachukiza, kikosa kueleweka,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
"Ukikopa kila mara, watakwita nyangarika"
Maneno haya hukera, lakini ya kweli kaka,
Yaweke kwenye fikira, usije kuabika,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
Kwa wote nilowakopa, kina dada kina kaka,
Na wote walionipa, msaada nilotaka,
Shukrani ninawapa, nawaombea fanaka,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
Kukopa mekuwa mwao, hawapendi kwa hakika,
Nimeona matokeo, vijana huhangaika,
Siseme shauri yao, wewe hayajakufika,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie,
Wataftaji wenzangu, lazima *tutaomoka,
Shahidi shairi langu, mwenyewe nimeandika,
Riziki hugawa Mungu, tutapata bila shaka,
Mwaka huu sitakopa, e Mola nisaidie.
Green Ruwa
Mtoto wa Gwiji
greenruwa@gmail.com
