Monday, November 20, 2023

BINTI YETU



BINTI YETU










Ni heri basi arudi, kuliko kututesea,

Kwa sasa hatuna budi, sisi kama familia,

Hizo dhiki zimezidi, mrudishe twakwambia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Kidato hakumaliza, kwa mimba ulompea,

Ukasema unaweza, mtoto kututunzia,

Nasi hatukukukataza, sharia tukafuatia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Amehangaika sana, binti yetu malkia,

Si usiku si mchana, watoto kuwatafutia,

Kisa wewe memukana, hutaki kusaidia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Hino ni simu ya saba, mtoto atupigia,

Kwa kesi za ukahaba, anazo kushtakia,

Japokuwa we ni baba, kwenye hio familia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Anakukosea wapi, mpaka watutesea,

Binti yetu ni wa dini, na anaheshima pia,

Amefunzwa tamaduni, hana mambo ya dunia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Wampiga kama fisi, hilo pia katwambia,

Tutahusisha polisi, ukome hizo tabia,

Ni heri aishi nasi, usije kutuulia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Basi waite wazazi, muje kutuelezea,

Mambo yako yawe wazi, tuweze kusamehea,

La sivyo hatuwezi, binti kukurudishia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

 

Twashkuru mumefika, kesi kuifuatilia,

Kijana wenu hakika, binti ametutesea,

Kiapa kubadilika, wazazi tutaridhia,

Binti yetu mrembo, huwezi kututesea

BINTI YETU

BINTI YETU Ni heri basi arudi, kuliko kututesea, Kwa sasa hatuna budi, sisi kama familia, Hizo dhiki zimezidi, mrudishe twakwambia, Binti ye...