Ni heri basi arudi, kuliko kututesea,
Kwa sasa hatuna budi, sisi kama familia,
Hizo dhiki zimezidi, mrudishe twakwambia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Kidato hakumaliza, kwa mimba ulompea,
Ukasema unaweza, mtoto kututunzia,
Nasi hatukukukataza, sharia tukafuatia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Amehangaika sana, binti yetu malkia,
Si usiku si mchana, watoto kuwatafutia,
Kisa wewe memukana, hutaki kusaidia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Hino ni simu ya saba, mtoto atupigia,
Kwa kesi za ukahaba, anazo kushtakia,
Japokuwa we ni baba, kwenye hio familia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Anakukosea wapi, mpaka watutesea,
Binti yetu ni wa dini, na anaheshima pia,
Amefunzwa tamaduni, hana mambo ya dunia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Wampiga kama fisi, hilo pia katwambia,
Tutahusisha polisi, ukome hizo tabia,
Ni heri aishi nasi, usije kutuulia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Basi waite wazazi, muje kutuelezea,
Mambo yako yawe wazi, tuweze kusamehea,
La sivyo hatuwezi, binti kukurudishia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea
Twashkuru mumefika, kesi kuifuatilia,
Kijana wenu hakika, binti ametutesea,
Kiapa kubadilika, wazazi tutaridhia,
Binti yetu mrembo, huwezi kututesea





